Zaidi ya watu 3,000 wanaodaiwa kuuziwa ardhi ya kanga iliyokuwa ikichimbwa saruji na kampuni ya East Africa Portland katika eneo la Athi River Kaunti ya Machakos, wanalaumu Idara ya Polisi katika Kaunti hiyo kwa kutumiwa na mabwenyenye wanaotaka kupora ardhi hiyo kuwahangaisha.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa muungano wa Kadhama Welfare Association Peter Mwandia, wakaazi hao wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati kwani wanahisi huenda kuna ufisadi mahali.

Mwandia alidai kuwa kuna mtu ambaye ameungana na Kamanda wa Polisi wa Utawala katika Kaunti hiyo Joseph Keitany na kufurusha wananchi ambao waliahidiwa na kampuni hiyo ya saruji kuwa watauziwa hilo shamba.

Wakaazi hao walikuwa wakizungumza na Waandishi wa Habari mjini Athi River katika Kaunti ya Machakos asubuhi ya leo (Ijumaa).

Wakati uo huo akina mama wakongwe pia walidai kuwa Polisi wamekuwa wakiwahangaisha bila sababu yoyote ya kuwahangaisha.

Mwenyekiti wa shirika la Syokimau Mavoko Association Pius Musembi ametishia kuelekea Mahakani kuchukua amri za kuwazuia Maafisa wa Polisi kuingia kwenye ardhi hiyo yenye zaidi ya ekari 3,300.

hata hivyo, Kamanda Keitany amepuuzilia mbali madai hayo na kusema kuwa wanaodai hivyo ni watu wanaotaka kumchafulia jina kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Keitany amedai kuwa Maafisa wa Polisi hufika kwenye eneo hilo kudumisha usalama kwani ardhi hiyo ingali chini ya kampuni ya saruji ya East Africa Portland.