Wakaazi wa kijiji cha Bondonya, katika lokesheni ya Bassi Masige, eneo bunge la Bobasi wamelalamikia ongezeko la fisi katika eneo hilo, haswa nyakati za usiku.

Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wakaazi ambao waliongea na mwandishi huyu walidai kuwa mbuzi watatu waliliwa mwezi wa tatu na kile wanachoshuku kuwa fisi.

Pia waliongezea kuwa pamesikika mlio wa mnyama huyo hatari haswa nyakati za usiku, huku wakidai kuwa si fisi mmoja, bali inaonekana wako zaidi ya mmoja na watoto wake.

Naomi Kerubo, ambaye mbuzi wake mmoja aliliwa na mnyama huyu mwanzo wa mwezi Aprili, alidai kuwa fisi hao wamekuwa wakitembea usiku na kutoa milio mikali, jambo ambalo limemtia wasiwasi mkubwa.

“Kwa wiki tatu sasa kumesikika milio ya fisi ambaye inaonekana kuwa na watoto sasa hakuna kuenda dukani usiku,” alisema Kerubo.

Naye Samuel Onsarigo, ambaye ni msaidizi wa Naibu chifu katika kijiji hicho alithibitisha madai hayo akikubali kuwa yeye ni mwaathiriwa kwani mbwa wake wawili walipapurana wiki jana ambapo mmoja wa mbwa alijeruhiwa vibaya katika mguu wa mbele kushoto.

Hata hivyo, Onsarigo alisema kuwa hii si mara ya kwanza fisi kuwepo katika kijiji hicho, kwani ni kawaida ya wanyama hao kuonekana haswa msimu huu wa miwa ikiwa mikubwa fisi upenda kujificha ndani.

Hawa fisi wamekuwa tangu nyuma, hasa miwa inapokuwa mikubwa na hapa kwetu tuna miwa hasa hii ya kutengeza sukari nguru ambayo inakuwa kama msitu ambamo wanyama hawa ujificha,” aliongeza mkazi huyo.

Naye Naibu chifu wa eneo hilo John Morang'a alisema amesikia tu kutoka kwa mkaazi mmoja ambaye mbuzi wake alivamiwa na kuliwa na mnyama anayeshuku kuwa fisi.

Naibu huyo alishauri wakaazi hao kufungia mifugo yao katika nyumba na wakome kuacha mifugo nje.

Pia aliwataka wanakijiji hao angalau kuwa na mbwa mmoja kila boma kwani fisi akisikia mbwa akibweka huogopa.

“Mbwa ni muhimu katika kila boma, fisi na mbwa ni maadui na hakikisha mifugo wanafungiwa zizini," alishauri wakazi huku akiwasihi wakulima walio na miwa ya sukari nguru kukoma kupanda karibu na makaazi yao na iwapo ni lazima, wawe na mbwa ambao wataweka usalama katika boma.