Wakaazi kutoka eneo bunge la Bomachoge Chache kaunti ya Kisii wamelalamikia barabara mbovu ya kutoka eneo la Ogembo kuelekea eneo la Nyamasege .
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne wakazi hao wakiongozwa na zablon Mekenye walisema barabara hiyo imekuwa mbaya na hakupitiki kamwe na kumwomba mbunge wa eneo bunge hilo la Bomachoge chache Simon Ogari kuweka barabara hiyo lami ili wananchi wa eneo hilo wafaidike.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya wanabodaboda wa eneo hilo kuandamana na kupanda migomba katika barabara hiyo, jambo ambalo wameapa kuwa hawatawacha mpaka hatua ichuliwe na barabara kutengenezwa.
“Tunaomba barabara hii itengenezwa haraka kwasababu wananchi wa eneo hili wanasumbuka sana hasa wakati mvua inaponyesha. Hatua ya kukarabati barabara hii ichukuliwe haraka kwani viongonzi walichaguliwa kufanya maendeleo,”alisema Mekenye, mkaazi wa eneo hilo.
Wakati huo huo, wakaazi hao waliomba daraja lililo katika eneo la Ogembo ambalo limeonekana kuharibika likarabatiwe pia ili kuruhusu wanachi kupita katika eneo hilo.
“Wananchi wanaogopa kupita katika Daraja hili la Ogembo maana limeharika na kuwalazimu wananchi kutumia njia mbadala ambayo ni ndefu. Tunaomba wahusika waonyeshe uwazi na huruma kwa wananchi wa eneo hili kwa kukarabati daraja hilo ambalo kwa sasa ni hatari kwa maisha ya watu ambao wanatumia barabara hiyo,” alisema Charles Ogembo, mkaazi wa eneo hilo.