Wenyeji wa eneo bunge la Bomachoge chache walipokea matibabu na kufanyiwa uchunguzi bila malipo katika kituo cha afya cha Egetonto kwa ufadhili wa mzaliwa wa eneo hilo anayeishi marekani, Job Nyangenya.
Zaidi ya wenyeji 1,000 walijitokeza siku ya Ijumaa kushiriki matibabu na uchunguzi huo, huku wauguzi wazaliwa kutoka eneo hilo wakijitolea kufanikisha mpango huo kwa ujuzi wao kwa msingi wa shirika lisilo la kiserikali la ‘Health rescue centre’.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Roseline Nyakona, idadi kubwa ya watu waliojitokeza inaashiria jinsi ambavyo wenyeji wanapitia shida kuhusu magonjwa mbalimbali, na hasa walio mbali na vituo vya afya.
“Tangu asubuhi tumekuwa tukipokea walio na shida mbalimbali tukiwapa matibabu, mawaidha ya kiafya na jinsi ya kijikinga na baadhi ya maradhi mengine,”alisema Nyakona.
Mfadhili asilia wa mpango wa kuwahakikishia afya bora watu wa eneo bunge la Bomachoge chache Job Nyangenya amekuwa katika mstari wa mbele kuendeleza warsha za kuwahamasisha wenyeji kuhusu afya, kando na kufadhili mpango wa teknolojia za kisasa katika shule zilizoko katika eneo hilo.
Wakati uo huo, viongozi mbalimbali walionyesha furaha yao kuhusiana na mpango huo, huku wakisema kuwa huu unafaa kuwa mfano kwa kila mzaliwa wa eneo bunge hilo kuanzia mbunge hadi wawakilishi wa wadi.
“Hili ni jambo la busara sana ambapo wakaaji wa mashinani wanapata jukumu la kufanyiwa uchunguzi wa kiafya kando na kupokea matibabu ya bure,” alisema Samson Maoto, aliyekuwa mwakilishi wa wadi katika eneo la Misesi.
Magonjwa ya kawaida yalishughulikiwa, yale yasingethibitiwa waliougua walielekezwa katika hospitali spesheli.
Mkurugenzi wa shirika lililofanikisha mpango huo alisema kuwa kusubiri hadi magonjwa yazidi watu ndilo jambo la hatari kwa afya, huku akiwataka wafanye mazoea ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa kila mara kuepusha athari mbaya.