Wakaazi wa tarafa ya Elburgon wameitaka wizara ya ardhi kutoa hatimiliki za mashamba katika eneo hilo, kama njia moja ya kutatua mizozo ya ardhi.
Wakaazi wa eneo hilo wamelalama kuwa yaliyokuwa mabaraza ya miji yaliwauzia wakaazi ploti bila kutoa stakabadhi muhimu za umiliki.
Wamesema ploti pamoja na mashamba katika eneo hilo hazina hatimiliki, wakisema mizozo ya ardhi imepelekea migogoro kati ya wakazi mjini humo.
Mwenyekiti wa wafanyibiashara katika eneo la Elburgon Joseph Kahura amesema tatizo la kipande kimoja cha ardhi kumilikiwa na zaidi ya watu watatu si jambo geni katika eneo hilo.
Amesema baadhi ya maafisa wa yaliyokuwa mabaraza ya miji waliuza ploti kwa mbinu fisadi, jambo ambalo linachangia mizozo ya umiliki wa ploti.
Mwakilishi wa Wadi ya Elburgon Florence Wambui ameuliza serikali kusitisha uuzaji wa ploti katika kaunti ya Nakuru, hadi pale mizozo iliyopo itakapotatuliwa.
Amesema ni sharti wakazi wa Elburgon wapewe ramani rasmi ya mji huo kama hatua ya kwanza ya kutatua changamoto za umiriki wa ardhi.
Wamesema ukosefu wa hatimiliki ni changamoto kubwa kwa wakaazi, huku wakiongeza kuwa miradi ya maendeleo kama vile kuwekwa kwa nguvu za umeme pamoja na maji hutekelezwa katika mashamba ambayo yanatambulika kisheria.
Aidha, imetambulika kwamba ghasia zilizozukua nchini kati ya mwaka 92 hadi 2007, zilitatiza uchumi wa Tarafa ya Elburgon, huku wakazi wengi wakiishi kama maskuota.