Wakaazi wa Isamwera, katika Kaunti ya Kisii wanahitaji mafunzo maalumu jinsi ya kukabiliana na funza ambao wamewaathiri watu wengi katika eneo hilo.
Akiongea hii leo na mwadishi huyu katika lokesheni ya Isamwera, chifu Nelson Omae amewaomba wahudumu wa sekta ya afya kutembelea wakaazi hao na kutoa mafunzo maalumu jinsi ya kukabiliana na funza ambao wamewaathiri wakaazi wengi katika eneo hilo.
“Naomba wahudumu wa afya kutembea katika lokesheni yangu ili kutoa mafunzo maalumu jinzi ya kukabiliana na funza,” alihoji Chifu Omae.
Kulingana na chifu huyo, watu wengi wameathirika na funza, hasa watoto wachanga ambao husumbuliwa na funza hao, ambao wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wahudumu hao.
Kwa upande wa wahudumu wa afya hasa wa Jamii, wako tayari kuenda katika eneo hilo ili kuwasaidia wakazi hao hasa watoto wadogo ambao hawaendi shule kutokana na kuathiriwa na makali ya funza .
Mhudumu wa afya ya Jamii katika kaunti ya Kisii Kepha King’oina amesema kuwa wanaendelea kutafuta siku ambayo watatembelea maeneo hayo hili kuwasaidia wakazi hao na kuwaomba wazazi kushirikiana nao wakati wataenda katika eneo hilo, hii ni baada ya maafisa hao kuenda eneo hilo hapo awali na kukosa ushirikiano mwema kutoka kwa wakazi hao..
King’oina amewaomba washikadhau wengine kujitolea hili kuwasadia wakazi hao, huku akisema kuwa kuna watoto katika maeneo hayo ambao wanahitaji msaada wa chakula ili waweze kupata madini.
“Ninaomba washikadhau na wahisani wema kujitolea ili kupiga vita funza haswa katika vijijini na kuanzisha mradi wa kupeana mafunzo jinsi ya Kukabiliana na janga hili,” alihoji Kingoina.
Aidha, ameiomba serikali ya kaunti ya Kisii kushirikiana na sekta ya afya ili kutoa madawa ya funza yatakayosaidia wakazi hao.