Wakaazi kutoka eneo la Coke katika maskani ya Jogoo Estate viungani mwa mji wa Kisii wameiomba Idara ya Polisi katika Kaunti ya Kisii kuwahakikishia usalama wa kutosha katika eneo hilo.
Mwito huu umetolewa siku mbili tu baada ya mama mmoja ambaye anafanya na kiwanda cha kutengeneza Soda cha Coca-Cola kushambuliwa siku ya Jumapili asubuhi alipokuwa akielekea kazini ambapo alijeruhiwa vibaya katika miguu na kichwa.
Mmoja wa wakaazi hao ambaye alishuhudia kisa hicho Deborah Moraa, aliomba kutumwa kwa Maafisa wa Polisi kupiga doria katika eneo hilo ambalo alisema limekuwa baya hasa nyakati za asubuhi na usiku akiongeza kuwa ni chini ya mwezi mmoja ambapo anaye endesha Bodaboda alivamiwa na kuuwawa na majambazi kabla ya kupokonywa Bodaboda yake.
"Majambazi wamezidi kuvamia watu katika eneo hili hata muda wa asubuhi ya saa moja. Serikali ya Kaunti yetu na Idara ya Polisi sharti wazingatie usalama wetu kama wananchi wa Kenya,” alihoji Moraa.
Naye Charles Sawe ambaye ni mwendeshaji Bodaboda katika eneo hilo alisema kuwa wahalifu hao wameanza uvamizi huo baada ya eneo hilo kuanza kupangizwa na wanafunzi pamoja na wafanyikazi wa kampuni ya Coke huku wakidhania kuwa wengi wao wana pesa na bidhaa za thamani kama vile tarakilishi na simu aina ya ‘Smart Phone' ambapo huwapiga wapangaji hao na kuwaumiza wanapokosa kuwapa kile wanataka.
"Mimi ninapofika saa mbili siwezi kubeba mteja yeyote anayeenda eneo hilo kwa sababu wengine huwa wanajifanya abiria kumbe ni jambazi," alifafanua mwendesha Bodaboda huyo.
Naye mfanyabiashara mmoja ambaye alijitambulisha kama Mama Faith aliongezea kuwa imembidi kufunga duka lake mapema saa moja huku akihofia kuvamiwa na wahalifu hao ambao anadai wanalenga wafanyikazi, wanafunzi na wafanyibiashara.
Hata hivyo juhudi zetu za kuzungumza na Chifu wa eneo hilo ziligonga mwamba baada ya kumkosa kwenye simu yake.
Kisa hicho kilizua hasira miongoni mwa wakaazi ambapo waliwachapa na kuwafurusha vijana wawili ambao walihamia sehemu hiyo hivi majuzi ambao wanashukiwa kutokuwa na shughuli maalumu ya kuwapa mapato.