Wakazi wa eneo la KARI viungani mwa mji wa Kisii wametishia kufanya maandamano dhidi ya mwakilishi mmoja wa wadi kutoka kaunti ya Nyamira, kwa madai ya kuvunja muundo msingi wa majitaka.
Wakaazi hao, wakiongozwa na mmoja wa wamiliki wa nyumba katika eneo hilo Nancy Aoko, ambaye nyumba yake imewahi kugongwa na gari la mwakilishi huyo na kuporonoka kwa upande mmoja, alidai kuwa bomba la majitaka limevunjwa zaidi ya mara tano na magari ya mwakilishi huyo, ambayo husafirisha bidhaa za kujengea kama simiti na mawe ya nyumba yake inayoendelea kujengwa kwa sasa.
Wakaazi hao ambao walikuwa wameanza kuandamana na baadaye kusitisha maandamano hayo kufuatia ushauri kutoka kwa mmoja wa kiongozi kutoka sehemu hiyo kuahidi kushughulikia swala hilo, waliiomba serikali ya kaunti ya Kisii kuingilia kati ili kutatua shida hiyo haraka iwezekanavyo.
“Wengine wetu tuna watoto wadogo ambao huchezea hapo nje; hii 'siweji' huenda ikawadhuru kiafya na kutusababishia magonjwa sisi kama wakaazi wa sehemu hii,” alisema Mama Mary Arasa, ambaye ni mmoja wa wale wanaoathirika zaidi kwani seweji hiyo iko karibu na mlango wake.
Hata hivyo hii si mara ya kwanza wakaazi hao kulalamikia swala hilo la mabomba ya majitaka kuvunjwa na kuvuja kuenda milango ya watu.