Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika la msalaba mwekundu kaunti ya Nakuru linazidi kuwahimiza wakaazi kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam kuhusu athari za mvua ya El Nino ambayo inashuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akiongea na mwandishi huyu kwa njia ya simu, jumamosi, meneja wa shirika la msalaba mwekundu kaunti ya Nakuru, Emmanuel Owako amewataka wakaazi kuchukua tahadhari hizo licha ya sehemu zote kutoshuhudia kiwango kikubwa cha mvua.

Alisema tayari, watu wanaoishi katika nyanda za chini wamehimizwa kuhamia sehemu za juu kutokana na mafuriko, akiongezea kuwa maeneo ya Solai na Mau hivi karibuni yalishuhudia maporomoko ya ardhi.

“Ingawa baadhi ya maeneo hayajashuhudia mvua hiyo ya El Nino, huenda mvua hiyo ikanyesha hivi karibuni na kutokana na hadhari hiyo, watu wanafaa kujiandaa kikamilifu. 

Katika eneo la Solai, jamii inayoishi hapo imeshauriwa kuhamia maeneo ya nyanda za juu,” alisema Owako.

Meneja huyo aidha ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana ili kuzuia athari zaidi za mvua hiyo kwenye kaunti ya Nakuru.

“Tunahimiza wadau kuungana pamoja ili tuweze kushirikiana kuzuia madhara ambayo huenda yakatokana na mvua ya El Nino. Nawahimiza washirikiane katika kuwapasha wananchi habari kuhusiana na El Nino ili jamii isiweze kuadhiriwa," aliongeza Owako.