Mkurugenzi wa shirika lisilo la serikali la Ecumenical Centre for Justice and Peace (ECJP) Johnson Ingor ametoa wito kwa wakaazi wa Kaunti ya Kisumu kutumia vyema uhuru wa katiba mpya ili kua na amani thabiti miongoni mwao.
Ingor ambaye ni mwenyeji wa German na ambaye yupo nchini kwa mwaka wake wa tatu kwenye zamu yake ya muhula mmoja wa miaka mitano, aliwasihi wakaazii wa eneo hilo kupata usaidizi kutoka ofisi zote za kila idara katika Kaunti hiyo kupitia kwa viongozi wao walioteuliwa.
Akiongea kwenye ofisi ya shirika hilo katika Tawi la Kisumu ilioko eneo la Daraja Mbili siku ya Jumamosi asubuhi, Ingor aliwataka wakaazi wa Kaunti hiyo kutumia vyema mtandao ulioanzishwa eneo hilo wa, SMS Platform unaotumia simu za rununu kwa huduma ya ujumbe mfupi raia kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa Kaunti hiyo.
“Tunahitaji kila mwananchi aweze kupata usaidizi wakati wowote bila dhuluma. Pia tunataka mwananchi naye kutumia uhuru huo kwa njia stahiki ili kuwepo na manufaa ya maendeleo na amani thabiti kwetu sote kama nchi na taifa,” alisema Mkurugenzi Ingor.
Mtandao huo ulizinduliwa mnamo mwaka uliopita kwenye Kaunti hiyo ambayo ililengwa katika eneo la Magharibi miongoni mwa maeneo ambayo yaliathirika pakubwa na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Shirika hilo la ECJP linalofanya kazi yake kupitia kwa viongozi wa makanisa, linaongoza katika mstari wa mbele kupigania haki za kibinadamu, wakati linapoendeleza kampeni za kuelimisha wananchi kuhusu haki zao na utangamano miongoni mwao pamoja na uongozi bora kupitia elimu ya urai.