Wakaazi wa kijiji cha Mobamba Wilayani Kebirigo, Kaunti ya Nyamira wamewaomba Maafisa wa Polisi kuingilia kati ongezeko la utengenezaji wa pombe haramu ambao wamedai umekita mizizi katika eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongea na Mwandishi wa Habari huyu siku ya Ijumaa katika kijiji hicho cha Mobamba, wakaazi hao walilalamikia ongezeko la biashara ya pombe haramu katika sehemu hizo na kuomba Maafisa wa Polisi kuingilia kati ili kuikomesha.

“Tumeshindwa jinsi ya kukomesha upikaji wa pombe katika sehemu hizi. Biashara hii ya pombe imepelekea kuvunjika kwa ndo nyingi kupitia unywaji wa pombe kwa baadhi ya wanaume katika eneo hili na kuwasahau familia yao, jambo ambalo linakera mno,” alihoji Jackline Bochaberi mkaazi wa kijiji cha Mobamba.

Wakaazi hao walikiri kuwa ulevi wa pombe katika eneo hilo umeharibu vijana wa umri mdogo na hata kusababisha baadhi ya vijana kukosa kuenda shule huku boma za watu wengine zikivunjika kwa sababu ya unywaji huo wa pombe.

“Hatuwezi kufurahishwa tukiona ndoa za wenzetu zikifunjika, mimi mwenyewe mke wa ndugu yangu analia kila wakati kuwa mzee anarejea nyumbani usiku, mara haji kwa nyumba, wala hapeleki chochote nyumbani. Suluhu ya mambo hayo ni pombe kukomeshwa kabisa katika eneo hili,” alisema Kevin Nyakundi mwanakijiji cha Mobamba.

Wakati uo huo, wakaazi hao waliapa kuwa kama Serikali haitaingilia kati suala hilo kikamilifu na kulishughulikia kwa haraka, basi huenda wao wenyewe waanze kufanya msako nyumba baada ya nyumba na kuhakikisha wagema kutopika pombe hiyo ya haramu.

Baadhi ya wakaazi walisema machifu wa eneo hilo wanajua wagema ambao wanafanya biashara hiyo, lakini kulingana nao, hawajawahi onyesha dalili ya kuwakomesha kupika pombe hiyo ya haramu.

Wakaazi hao walisema kuwa ni siku mbili tu zimepita tangu mwendesha Bodaboda mmoja adungwe kisu tomboni na kufariki katika nyumba ya pombe katika kijiji hicho na kuwapelekea wengi kuogopa kuwa watu wengi zaidi huenda watakufa.

“Hata sisi wenyewe tunaweza kuwakomesha wanaofanya biashara hii haramu kama Machifu na Maafisa wa Polisi watakawia kuwachukulia hatua wagema hawa ambao hawataki kufuata sheria iliyowekwa kuwa pombe haramu isitengenezwe,” aliongezea Nyakundi.