Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi wa eneo la Khadija katika Kaunti ya Mombasa wamesisitiza kuwa hawatakubali kuondolewa katika eneo hilo ili kupisha ujenzi wa nyumba mpya za kisasa.

Wakaazi hao wanadai kwamba Gavana wa kaunti hiyo Hassan Joho aliwaagiza kuondoka sehemu hiyo ifikiapo mwezi April mwaka huu, ili watoe nafasi ya ujenzi huo wa ghorofa.

Wakiongea na wanahabari katika shule ya msingi ya Khadija siku ya Jumamosi, wakaazi hao walimshtumu gavana kwa kushinikiza swala hilo wakiongeza kuwa hawana sehemu nyingine ya kwenda.

“Gavana Joho anasema anataka kuvunja hizi nyumba zilizoko hapa ili kujengwe ghorofa za kisasa. Sisi wakaazi hatujahusishwa katika mpango huo na hatuoni kama ni haki kabisa,” alisema Hassan Abubakar, mkaazi.

Inadaiwa kuwa wakaazi hao waliagizwa kuwa mwezi Machi ndio mwisho wa kulipa kodi za nyumba wanazoishi ili ifikiapo mwezi Aprili ubomozi uanze.

Waliongeza kuwa Gavana Joho aliwaahidi kuwa watapewa fidia ya shilingi laki tano kila mmoja kabla kuondoka katika nyumba hizo, jambo wanalopinga huku wakimlaumu Joho kutokana na uamuzi huo.

Sasa wanaitaka serikali ya kaunti kusitisha mpango huo huku wakiongeza kuwa hawataweza kumudu gharama ya nyumba hizo mpya zitakazojengwa, kwani itakuwa ghali mno ikilinganishwa na zile wanazoishi kwa sasa ambapo wanalipa shilingi elfu tatu kwa mwezi.

Eneo hilo la Khadija Estate lina zaidi ya nyumba 100 na sasa wakaazi hao wana hofu kwamba maisha yao yatakuwa taabani watakapoondolewa sehemu hiyo huku wakitaja mradi huo wa kujenga ghorofa kama usio na manufaa kwao.