Wakaazi wa eneo la Kiogoro lililoko eneo bunge la Nyaribari Chache wamefurahi na kushukuru serikali ya kitaifa kwa kuweka matuta kwa barabara  kuu ya kutoka Kisii kuelekea Kilgoris, ambapo ajali nyingi zimekuwa zikitokea kila mara.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongea na wanahabari katika eneo hilo la Kiogoro, wakaazi hao walishukuru serikali ya kitaifa kwa kusikia kilio chao baada ya maisha ya watu wengi kuwa hatarini, huku wengine kupoteza maisha katika eneo hilo kupitia ajali za barabara.

“Tunashukuru serikali kuu kwa kutimiza ahadi ambayo ilikuwa imetoa baada ya mbunge wetu Richard Tong’i kuomba wizara ya uchukuzi kutuwekea matuta ili waendeshaj wapunguze mwendo wa kasi wanapoendesha magari,” alihoji Gladys Osiemo, mkaazi.

Mbunge huyo alipeleka malalamishi ya kuweka matuta kwa barabara hiyo kwa wizara ya uchukuzi nchini hapo mbeleni, kwa kuiomba wizara hiyo kuweka matuta kwa barabara hiyo jambo ambalo sasa limeshughulikiwa kikamilifu.

Ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika barabara hiyo kwa mda mrefu, jambo ambalo liliwapelekea wakaazi wa eneo hilo kujiwekea matuta ya mchanga, na sasa wamewekewa matuta halisi.

Madereva na wanabodaboda wameombwa kupunguza mwendo wanapoendesha  ili kulinda maisha yao katika eneo hilo.

Kwa upande wa wakaazi hao, walishukuru serikali kwa kuwakumbuka na kusema sasa wamepata afueni kubwa kwa maisha yao.