Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Watu wanaoishi na ulemavu pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta tawi la kisii, wameanzisha msafara wa kuhamasisha uma kuhusu maswala ya jinsia na ulemavu.

Wakiongozwa na baadhi ya watu wanaoishi na ulemavu Kisii, wanafunzi hao walienda katika maeneo tofauti ili kuhamasisha wakaazi wa mji wa kisii na viungani mwake kuhusu swala la jinsia na ulemavu na changamoto zinazowakumba wake kwa waume na watoto wa jinsia zote kwa jumla kote duniani.

Akiongea katika hafla hiyo katika uwa wa Gusii siku ya Ijumaa, Bwana Issac Rogito, ambaye ni kipofu kutoka ofisi ya chama cha kitaifa cha walemavu mjini kisii, aliwaomba wakaazi wa mji wa kisii kusaidia walemavu wanapohitaji msaada wao.

"Ulemavu si kupenda kwa mtu, ni mapenzi yake mungu na basi nawaomba muwasaidie watu wanaoishi na ulemavu wanapowajia kwa msaada wowote. Wazazi wapelekeeni watoto wenu walio na ulemavu shuleni ili wapate mafunzo yatakayo wasaidia katika siku za usoni," alisema Rogito. 

Aidha, Fredrick Nyabando wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta tawi la Kisii, aliwaambia wakaazi hao kuwa ulemavu huwezi zuia mtu kufanya yale mungu anamtaka ayatende. 

Aliomba wakaazi kuwasaidia walio na ulemavu na kuwaomba wanaume kujitokeza ili pia nao shida zao ziweze kutatuliwa. 

"Wanaume tusiwe na kasumba ambazo hupelekea sisi kuumia bila wakutusaidia. Nawaomba kujiunga na kundi la kutetea haki za waume ili mupate msaada munapokua na machangamoto za kijinsia au ulemavu," alisema Nyabando.

Kilele cha msafara huo kilikua na michezo tofauti katika uwa wa Gusii ikiwemo mpira wa nyavu na kandanda. Washindi walizawadiwa vyeti.