Wakaazi wa mji wa Kisii wameiomba sekta ya uchukuzi katika kaunti hiyo kushughulikia suala la msongamano wa magari katika mji wa huo.
Wakiongea siku ya Alhamisi katika barabara ya daraja moja kuelekea kituo cha magari mjini Kisii, baadhi ya wakaazi wameiomba sekta ya uchukuzi kuweka mikakati kabambe ya kusaidia kutoa msongamano ambao unashuhudiwa katika mji wa Kisii hasa siku za soko.
“Tunaomba sekta ya uchukuzi ikishirikiana na wasimamiza wa kaunti ya Kisii kushughulikia suala hili kwani wakati wa msangamano biashara husimama,”alisema Hennel Bogonko, mfanyibiashara.
Aidha,wakaazi hao walisema kuwa siku ya Jumatatu hushuhudiwa msongamano mkubwa kwa kuwa siku hiyo ni ya soko la Daraja mbili na watu wengi hutoka maeneo mbalimbali ili kuja kufanya biashara katika soko hilo.
Wakaazi hao waliongezea kuwa msongamano hushuhudiwa siku ya Alhamisi kutokana na watu kufika katika chumba cha kuhifadhi maiti ili kuwachukua wenzao waliofariki.
Kwa sasa wakaazi hao wameiomba sekta hiyo kuweka mikakati kabambe kwa kuwa barabara za mji wa Kisii hazipitika wakati wa msongamano huo na kuiomba serikali ya kaunti kupanua baadhi ya barabara hizo.
“Serikali ya Kaunti ya kisii ikishirikiana na sekta ya uchukuzi inastahili kupanua baadhi ya barabara kwa kuwa watu wanaendelea kujaa katika mji wa Kisii,”alisema Jimmy Osoro, mwendeshaji bodaboda.
Baadhi ya Barabara ambazo huwa na msongamano mkubwa ni barabara ya Daraja mbili-Daraja moja, barabara kutoka hospitali ya Kisii kuelekea Mashauri, na barabara ya Daraja moja kuelekeaTuskys.