Wakaazi wa kaunti ya Kisii wamehimizwa kupanda miti kama njia moja ya kutunza mazingira.

Share news tips with us here at Hivisasa

Pia wameshauriwa kuhakikisha kuna usafi kila mahali ili kuepukana na mkurupuko wa magonjwa kama vile kipindupindu.

Akiongea mnamo siku ya Ijumaa katika shule ya msingi ya Kisii wakati wa kuadhimisha siku ya mzingira ulimwenguni, msimamizi wa hotel ya Ufanisi Isabellah Lumumba alisema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa ametunza mazingira.

Lumumba pia aliiomba serikali ya kaunti ya Kisii kuwa katika msitari wa mbele katika upanzi na uhifadhi wa mazingira,

“Ni juku letu sisi kuhakikisha kuwa mazingira yetu ni safi na tupande miti kwa wingi. Aidha, tunafaa kuepukana na upanzi wa miti ambayo inaweza kuangamiza chemichemi za maji,” alishauri.

Lumumba aliihimiza kuelimishwa kwa watoto kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ili wanapokuwa wawe wanafahamu maana ya uhifadhi wa mazingira.

Hoteli ya Ufanisi ilipanda miche elfu kumi katika hafla ya siku hiyo ya mazingira ulimwenguni, na kuwaomba viongozi na wakaazi wa Kisii kujitokeza na kupanda miti katika siku ya mazingira kama njia moja ya kujiweka katika hali nzuri kimaisha.

Aidha, serikali ya kaunti ya Kisii haikuadhimishi siku hiyo kwa kile kilichosemekana kuwa ukosefu wa mpango maalum.

Hapo awali, ilikuwa imeratibiwa kuwa upanzi wa miti ungefanyika katika sehemu ya Igare iliyoko eneo bunge la Nyaribari Chache kabla ya kutupiliwa mbali.