Huku siku ya kuadhimisha siku ya maleria ulimwenguni ikikaribia, wakazi wa Kaunti ya Kisii wameombwa kutumia neti za kuzuia mbu ili kukomesha uambukizaji wa maradhi ya maleria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea na wWaandishi wa Habari hii leo Alhamisi, Dkt. Beatrice Kemunto ambaye anasimamia kitengo cha kudhibiti maleria katika Wizara ya Afya alisisitiza umuhimu wa kutumia neti hasa katika msimu huu wa mvua ambayo alisema huwa ni chanzo kikuu cha kuzaana kwa umbu ambao husababisha ugonjwa wa maleria.

"Nawaomba watu wote watumie neti kila wanapolala ili kujikinga na umbu ambao ni wengi msimu huu wa mvua nyingi nchini hasa kina mama wajawazito,” alishauri Dkt. Kemunto.

Alidokeza kuwa siku hiyo humu nchini itasherehekewa kwenye Kaunti ya Busia, ambapo aliomba wahudumu wa kijamii kutoka kila Kaunti kuwasiliana na wakuu wa afya wa Kaunti zao ili wafahamishwe eneo ambalo watafanyia hafla hiyo.

Alipendekeza pia kwa wakazi kuzoa na kufungulia maji yaliyodimbuka karibu na makazi kwani maji hayo huwa mahali pa umbu kuzaana.

"Komesha vidimbwi vya maji karibu na mahali mnakaa, pia hakikisha hakuna misitu karibu na nyumba zetu kwani hapo ndio umbu wanajificha na kueneza ugonjwa wa maleria,” alishauri Dkt. Kemunto.

Siku ya kuadhimisha maleria itasherehekewa mwezi Aprili 25 siku ya Jumamosi na kila Kaunti itaandaa maadhimisho hayo kwenye eneo maalum ambalo washirikishi wa afya wa kila Kaunti husika watawafahamisha wakaazi wa maeneo hayo.

Eneo la Nyanza na sehemu za Magharibi ya Kenya huwa na rekodi ya usambazaji wa ugonjwa huu wa maleria kulingana na takwimu za Wizara ya Afya na ile ya Shirika la Afya Duniani - WHO.