Wakaazi wa Kaunti ya Kisumu, wameonywa dhidi ya kula mizoga ya mifugo kutokana na maradhi mbali mbali inayotokana na nyama ambayo haiijapimwa.
Afisa Mkuu wa Mifugo katika Kaunti ya Kisumu Waga Jalang’o, alisema kuwa ni hatari kwa mtu yeyote kula nyama ya mbuzi, kondoo, ngurwe au ng’ombe anayefariki kutokana na maradhi.
“Visa vya watu kula nyuma ya mifugo wanaofariki katika mazingira ya kutatanisha vinazidi kuripotiwa katika eneo hili. Hatua hiyo ni hatari kwa afya ya yeyote anayefanya hivyo,” alionya Jalang’o.
Afisa huyo anasema kuwa mizoga ya mifugo inafaa kuzikwa, baada ya kufanyiwa uchunguzi na afisa wa idara ya mifugo.
Alitoa wito kwa wananchi kuripoti visa vya mifugo yao kufariki, badala ya kunyamaza na kisha kuamua kula nyama ya mifugo hao.
Jalang’o alisema kuwa ugonjwa wa kuhara, ni miongoni mwa magonjwa ambayo yanaathiri zaidi mifugo hasa msimu huu wa mvua.
Afisa huyo wa mifugo, alisema kuwa msimu huu wa mvua kubwa, kunaweza kuwa na viini ndani ya nyasi vinavyoweza kudhuru afya ya wanyama.
Alitoa changamoto kwa wananchi kuhakikisha kuwa mifugo wao wanapokea chanjo, mara mbili kwa mwaka, ili kuwaepusha na magonjwa ambayo huvamia mifugo kila mara.