Wakaazi wa Miwani/ Kiboswa wameitaka Wizara ya barabara na ujenzi kuweka matuta barabarani na alama za barabara kwenye barabara ya kutoka Chemelili ikipitia Miwani kwenda Kiboswa eneo la Kisumu.
Wakaazi wa maeneo hayo waliomba Idara husika kuyachukulia kwa umuhimu mkubwa malalamishi yao ya mara kwa mara kuhusu ajali za pikipiki na magari zinazohusisha wanaotembea kwa miguu wakiwemo wanafunzi wanaovuka barabara hiyo wakienda shuleni.
Wakiongea kwenye mazishi ya kijana mmoja mwanafunzi ambaye alifariki kutokana na ajali baada ya kugongwa na pikipiki alipokua akitoka shule mnamo siku ya Jumatano wiki iliopita, wakaazi wa kijiji cha Oruba walitaka hatua ya dharura kuchukuliwa ili kupunguza ajali katika eneo la shule na soko.
“Tunaomba kuwekwa matauta barabarani na alama za kuvuka barabara katika kila eneo la shule na hata soko, ili kupunguza visa vya ajali za mara kwa mara ambapo watoto wetu wanamalizwa kwenye njia ya ajali,” alisema Chifu wa eneo hilo, Nelson Ogwang.
Ojwang alisema kuwa waendeshaji pikipiki wanapita barabara hilo kwa mwendo wa kasi sana ambapo hata mtu akitokezea ghafla hawezi kudhibiti mwendo na kuzuia hatari.
“Tunaomba pia Maafisa wa Trafiki kutusaidia kuweka vizuizi kwenye barabara hili ili kuyanasa magari yasiyo na vidhibiti mwendo ili kupunguza ajali hizi za mara kwa mara,” alisema Janet Olaka, mkaazi wa eneo hilo.