Wakaazi wa wadi ya Marani eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini kaunti ya Kisii wamelalamikia ongezeko la bei ya mahindi katika eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongea na mwanahabari huyu mnamo siku ya Ijumaa katika soko la Marani, wakaazi hao walisema kufuatia ongezeko la bei ya mahindi, huenda wakabiliwe na njaa kwa mda mrefu.

Wakati huo huo, wakaazi hao waliomba serikali kuu kuleta mahindi humu nchini kutoka nje ya nchi, ili kukabiliana na njaa ambayo imenukia katika maeneo hayo.

“Tulikuwa tunanunua mahindi kilo mbili kwa shillingi 50, leo bei hiyo imeongezeka mpaka shillingi 100. Badala ya kununua kilo nne kwa shillingi 100, nitanunua kilo mbili pekee, sasa tuende wapi ?” alilalama mmoja wa wakaazi.

“Tunaomba serikali kuu ilete mahindi kutoka nje ya nchi jinsi ilikiri hapo mapema kuwa itahakikisha wananchi hawatakabiliwa na makali ya njaa, serikali ikifanya hivyo hatutakuwa na la kuogopa kukabiliwa na njaa,” alihoji mkaazi mwingine.

 “Tumeogopa kuwa huenda tuanze kununua mahindi kilo mbili kwa zaidi ya shiillingi 200, kwani mahindi tulipanda kwa mashamba yetu yako mbali kukuwa , maana tulichelewa kupanda kufuatia msimu wa kiangazi ambao tulishuhudia kwa mda mrefu katika sehemu hizi zetu za kisii,” aliongezea mkaazi mwingine.

“Tunaomba serikali itusaidie kwa kutupunguzia bei hiyo ya mahindi kwani tutakufa na njaa hivi karibuni na hatuna pesa zitakazotuwezesha kununua mahindi hayo mpaka mahindi yetu ambayo yako shambani yakue,” aliongezea.