Wakaazi wa mtaa wa Casino mjini Molo wamelalamikia oparesheni ya polisi ambao walivamia eneo hilo baada ya mmoja wao aliyedai rushwa kutoka kwa hadaki la pombe haramu kupigwa na wananchi siku chache zilizopita.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katika msako uliofanywa na maafisa wa kituo cha polisi cha Molo, vijana na kina mama wasiokuwa na hatia walipigwa kitutu na kurejuhiwa vibaya.

Wakazi hao wamesema zaidi ya maafisa wanane wa polisi, na ambao walijihami kwa bunduki pamoja na rungu, waliingia katika kila boma na kuvuruga amani kwa kuwajeruhi waliokuwemo.

Hali ya wasiwasi imetanda usiku kucha katika mtaa huo, huku wakaazi wakiendelea kulalamikia maovu yaliyosababishwa na maafisa hao katili ambao wanaendelea kuwahangaisha.

Wakazi hao wamesema maafisa wa polisi huwatia nguvuni vijana na kina mama, na badala ya kuwafikisha katika kituo cha polisi, wao hudai rushwa kutoka kwa waliokamatwa, huku wale ambao hawana pesa za kununua uhuru wao wakipigwa bila huruma.

Afisa mkuu wa eneo la Molo Stephen Kabii akidhibitisha kisa hicho alisema afisi yake inachunguza madai hayo, baada ya wakazi hao kutoa malalamishi.

Baadhi ya vijana waliovamiwa na maafisa hao wanaendelea kupokea matibabu baada ya kupelekwa katika hospitali ya wilaya Molo.