Mkuu wa kaunti ndogo ya Naivasha Abraham Kemboi ametoa ilani kwa wakazi wa eneo hilo wawe waangalifu kutokana na watu wanaojifanya kuwa wafanyikazi wa shirika la reli nchini.
Kemboi amesema tayari maafisa wa polisi wanasaka kundi hilo la watu ambao wanadaiwa kuanza kukusanya pesa pindi tu Rais Kenyatta alipotangaza kuwa reli mpya ya Standard Gauge Railway itajengwa hadi mjini Naivasha.
Akiongea mjini Naivasha Jumatatu, mkuu huyo amewataka wakazi watoe ripoti kuhusu yeyote anayejifanya kuwa mfanyikazi wa reli nchini katika eneo hilo.
"Kuna watu wanazunguka wakitafuta watu wa kuchukua pesa hapa eti ili kufidia ardhi itakayotumiwa na mradi huo wa SGR, tafahdalini nawasihi mjiepushe," Kemboi alisema.
Huku hayo yakijiri, jamii ya wafugaji imeelezea wasiwasi kuwa huenda mradi huo ukaathiri maeneo wanakolisha mifugo wao.
Kiongozi mmoja Joseph ole Kishau amesema kuwa mradi huo japo kuwa utawasaidia wengi huenda ukawa na madhara ya kimazingira iwapo hautatekelezwa kikamifu.
“Vijana wa sehemu hii wanafaa kupata nafasi za kwanza za kazi pindi tu mradi huo utakapo ng’oa nanga eneo hili” Alisema ole Kisau.
Naye Simon Saitoti alisema: “Kuna msitu wa eneo la Namucha ambako reli hiyo itapitia na huenda miti tunayotoa dawa asili iharibiwe.”
Kiongozi wa wanawake Susan Ndiabati kwa upande wake amehoji kuwa wale wanaotengeza reli hiyo walifaa waweke daraja eneo hilo ili wafugaji wawe wakipitisha mifugo wao bila kuteseka.