Serikali kupitia wizara ya ardhi imetakiwa kuwapa wakaazi wa eneo la Ndimu kaunti ya Nakuru hatimiliki za mashamba kama njia moja wapo ya kupunguza mizozo ya umiliki wa ardhi.
Wakaazi wa eneo hilo wamesema mashamba mengi wilayani Molo hayana hatimiliki licha yao kuendelea kushinikiza wizara ya ardhi kuwapa stakabadhi hizo muhimu.
Wakiongea katika eneo la Ndimu jumamosi, wakaazi hao wamesema kukosa hatimiliki za mashamba kumewafanya kubaki nyuma kimaendeleo, huku wakisema kwamba huduma kama za usambazaji wa nguvu za umeme hazijawafikia.
“Hatuwezi hata kukopa fedha kutoka kwa benki ama kufanya miradi mingine ya maendeleo kwa sababu hatuna hati za kumiliki mashamba” akasema mama Nancy Mwangi
Aidha walisema wengine wao wamepoteza mabwana zao, lakini wanachohofia zaidi ni mzozo kama ulioikumba kampuni ya Kihiu Mwiri, na sasa wanataka tume ya ardhi nchini kuwategulia kitendawili hicho.