Wakaazi wa eneo la Nyabite Egesieri eneo Bunge la Mugirango Kusini Kaunti ya Nyamira wameiomba Serikali kuwawekea matuta barabara ya la Nyabite–Nyamira–Kisii ili kupunguza ajali mwendo wa kasi wa magari.
Wakizungumza na Mwandishi huyu wa Habari siku ya Jumanne katika eneo la Nyabite, wakaazi hao walisema barabara zote za eneo hilo zinastahili kuwekwa matuta ili kupunguza mwendo wa magari ambayo huendeshwa kwa kasi na kusababisha ajali.
Hii ni baada ya mtoto wa umri wa miaka tisa kugongwa na gari siku ya Jumatatu katika eneo la Nyabite Egesieri na kufariki papo hapo, jambo ambalo limewapelekea wakaazi hao kuiomba Serikali kuweka matuta barabarani.
“Tunaomba Serikali yetu kama inajali maslahi na maisha yetu watuwekee matuta kwenye barabara zetu,” alihoji Lydia Kebabe mkaazi wa Nyabite.
“Serikali isipotuelewa huenda watoto wetu wakufe wote kwenye ajali ya barabara. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa matuta yamewekwa katika barabara za eneo hili ili kupunguza mwendo wa kasi wa magari,” aliongezea Kebabe.
Katika sehemu hiyo ya Nyabite shule ni nyingi ambazo na Serikali sasa imetakiwa kuhakikisha wanafunzi wa shule hizo maisha yao hayamo hatarini.