Kamishema wa kaunti ya Nyamira Josphene Onung’a amewaomba wananchi kuunga mkono mradi wa Nyumba Kumi.
Akiongea siku ya Jumanne katika mji wa Nyamira, kamishena huyo aliwataka wananchi kuunga mkono mradi huo ili kuimarisha usalama katika eneo hilo.
“Mkitaka tuwe na usalama wa kutosha katika kaunti yetu sharti tuajibike vilivyo maana usalama huanza na mwananchi. Mradi wa nyumba kumi unasaidia pakubwa kila mtu amjue wanayeishi naye,” alisema Onun’ga.
Aliongezea: "Hata wale ambao wamepangisha nyumba katika kaunti hii sharti mjue yule mnaishi naye na hiyo itahakikisha kuna usalama katika kaunti yetu.”
Kwingineko kamishena huyo aliwaonya wazazi wanaokeketa watoto wasichana na kusema hiyo ni kukiuka sheria za Kenya.
kwa upande mwingine, gavana wa kaunti hiyo ya Nyamira John Nyagarama alisema wakaazi wa kaunti hiyo watapata huduma bora ya afya katika hospitali za kaunti hiyo.
Aliwaomba wakaazi wa enoe hilo washirikiane naye kufanya maendeleo.
Aidha Nyagarama alisema ameweka mikakati ya kujenga chuo kikuu katika kaunti hiyo ili wanafunzi kupata masomo ambayo yatawasaidia katika siku za usoni.
“Hivi karibuni ujenzi wa chuo kikuu utaanza kwenye kaunti hii na wanafunzi wetu wataanza kupata masomo hapa nyumbani,” alisema Nyagarama.