Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa Kaunti ya Kisii, Nyamira, Migori na Homa-Bay wameiomba Serikali kuongeza kiwango cha pesa cha maeneo ya ustawi ya Bunge (CDF) kutoka 2.5% hadi 10%.

Wakiongea siku ya Jumanne katika hafla ya kutoa maoni kwa tume inayosimamia pesa hizo kama CDF inastahili kusimamiwa na Serikali za Kaunti au Serikali Kuu katika ukumbi wa Michezo na utamaduni wa Kaunti ya Kisii, wakaazi hao waliomba Serikali ya kitaifa kuongeza asilimia hiyo kwa nukta 7.5 ili kuifikisha asilimia 10.

Wakiongea katika ukumbi huo, baadhi ya wakaazi hao walisema kuwa asilimia hiyo ikiongezwa, miradi nyingi itafanyika na kukamilishwa mapema bila ukosefu wa pesa.

“Naomba pesa za CDF Serikali Kuu kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 10 ili miradi katika maeneo bunge zifanyike na kukamilishwa bila kuachwa katikati,” alihoji Christine Okoti kutoka Migori.

Aidha, wakaazi hao walilaumu Serikali za kaunti kwa kutenga pesa nyingi kwa miradi ambazo zinastahili kutumia kiasi kidogo cha pesa kulinganishwa na pesa CDF inatenga kwa mradi fulani.

“Ni matumaini yangu kuwa Serikali Kuu ikiongeza asilimia hiyo hadi 10 kuna mengi yatafanyika katika maeneo bunge yetu ambayo Serikali za kaunti haziwezi kufanya hasa katika ujenzi wa barabara na wa shule miongoni mwa miradi nyingine,” allihoji Bonfance Ondieki kutoka Kisii.