Wanabiashara wa wadi ya Sensi, eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini wamekashfu kampuni ya nguvu za umeme kwa hitilafu za umeme kwa siku tano mfululizo katika eneo hilo.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika eneo la Sombogo, wakaazi hao walisema kuwa eneo hilo limekosa nguvu hizo za umeme kwa siku ya tano mfululizo, na kuwasababishia kupata hasara kubwa kwani wanategemea stima .
“Mimi ni fundi wa kutengeneza milango ya chuma na dirisha za chuma, wakati nguvu za umeme zimekosekana, biashara zangu husimama kwa mda mpaka nitafute njia mbadala ili kumalizia wateja wangu kazi zao,” alihoji mmoja wao.
“Kutumia kifaa kama vile genereta ni ghali mno kwangu, maana hutumia petroli nyingi na huwa gharama kwangu, naomba kampuni ya KPLC itukumbuke kama wanabiashara na kutuonyesha uwazi maana tunawalipa baada ya kutumia nguvu hizo,” aliongezea fundi huyo.
Aidha, fundi huyo aliongezea kuwa anapotumia kifanyiza hatengezi pesa inavyostahili, kwani anapata faida ndogo ikilinganishwa na wakati anatumia umeme.
“Inabidi ninaabiri pikipiki kuenda kununua petroli ili niweke kwa kifanyiza wakati nguvu za umeme haziko na nauli hiyo natumia kuleta mafuta tena ni hasara maana stima ingekuwa singepoteza hizo pesa,,” aliongezea.
Aidha, wakaazi wengine walikiri kuwa mawasiliano yao hukatishwa kwa ghafla, maana simu zinapoisha moto hakuna mbinu mbadala ya kuweka simu zao kwa moto, jambo ambalo wamekerwa nalo na kuomba kampuni ya umeme kulishughulikia kikamilifu na kujali maslahi ya wakenya wote kwa usawa.