Serikali gatuzi ya Nakuru imetakiwa kufungua zahanati ambayo imekuwa haitumiki licha ya kujengwa na kukamirishwa na lililokuwa baraza la mji wa Molo kabla ya uchaguzi uliopita.
Hospitali hiyo dogo iliyofanyiwa ukarabati kwa kima cha Sh 800,000 baada ya kuharibiwa wakati wa machafuko ya 2007 ilikusudiwa kuwafaidi wakaazi wa maeneo ya Sirikwa, Nyakinyua, Mau Summit, Kangawa miongoni mwa maeneo mengine katika eneo bunge la Kuresoi Kaskazini.
Wakaazi hao wakiongozwa na Jackson Nyambogo wamesema zahanati hiyo kwa sasa ni kama ganjo baada ya kuendelea kuharibiwa na watoto wanaoitumia kama mahali pa kuchezea.
Amesema wakaazi walikuwa na matumaini mengi kuona huduma za afya zimeletwa karibu nao lakini hadi sasa wanaendelea kutafuta huduma za matibabu katika hospitali za wilaya Molo na Kuresoi ambazo ziko mbali nao.
Mkazi huyo amesema kina mama wajawazito pamoja na watoto hukosa kufika katika vituo vya afya huku changamoto zingine zikiwemo hali mbaya ya barabara zikiadhiri utoaji huduma za matibabu.
Ametamatisha kwa kusema licha ya wizara ya huduma za afya kukabidhiwa zahanati hiyo miaka mitatu iliyopita hospitali hiyo dogo bado haijawahi kutumiwa ili kusaidia wananchi wa eneo hilo.