Wakaazi wa Wadi ya Bogetaori katika eneo Bunge la Bobasi wamelalamikia jinsi pesa za ustawi wa Wadi almaarufu Ward Development Fund (WDF) zimetumika.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongea na Mwandishi huyu leo (Jumapili) asubuhi, baadhi ya wakaazi hao wanahofia kufujwa kwa fedha hizo na hivyo kumtaka Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae kuingilia kati.

Wakaazi hao wanadai kuwa Mwakilishi wa Wadi hiyo Bonface Okenye hakutumia pesa hizo za matumizi ya mwaka 2013/2014 ipasavyo.

Miongoni mwa miradi ambayo wanatilia shaka na wanasema imerekebishwa badala ya kutengenezwa kulingana na bajeti ya pesa hizo ni chemichemi za mito na madarasa ya chekechea ambayo ilitengenezwa na Serikali za mitaa iliyopita.

“Pesa za ustawi wa Wadi zilinuia kufanya miradi kikamilifu wala sio kurekebisha ile ya Serikali za mitaa na kuweka mfukoni zingine,” alilalamika Isaac Oonge mkaazi wa Wadi hiyo.

“Tunamwomba Gavana Ongwae aingilie kati na kuchunguza matumizi ya fedha hizo,” alipendekeza Jeriah Kerubo, mkaazi mwingine.

Mwakilishi Okenye kwa upande wake amekana madai ya ufujaji wa fedha na kusema kuwa hajahusika kwa njia yoyote katika kupeana tenda za miradi mbalimbali ya Wadi hiyo.

“Kuna baadhi ya watu wanaonipaka matope na kunichafulia jina kuwa nimekula pesa za ustawi wa Wadi. Hayo ni madai tu kwani miradi hupeanwa na Serikali ya Kaunti wala sio mimi jinsi wakaazi wanafikiria,” alikana Mwakilishi Okenye.