Wakulima katika Wadi ya Marioshoni katika Jimbo la Nakuru wameitaka Serikali kufungua tawi la hazina ya kitaifa ya nafaka na mazao (NCPB) katika eneo hilo ilikuwawezesha wakulima kunufaika na mbolea pamoja na mbegu ambazo zinatolewa na Serikali kwa bei nafuu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi hao wamesema kuwa licha ya kutembea kwa mwendo mrefu hadi Elburgon ambako kuna tawi la NCPB, wengi wao hurejea nyumbani mikono mitupu bila kupata mbolea na mbegu hata baada ya kutimiza masharti yote.

Wenyeji hao wamesema eneo la Marioshoni ni moja wapo ya maeneo yanayotegemewa kwa ukuzaji wa vyakula tofauti tofauti wakisema kuwa wakulima wamepoteza Matumaini baada ya kukosa mbolea ya Serikali tayari kwa msimu wa upanzi.

Wakulima hao ambao wameitaka Serikali ya Jimbo la Nakuru kuchunguza utendakazi wa maafisa wa bohari la Elburgon, wamesema kuwa wanakadiria hasara kwani tangu mwishoni mwa mwaka jana bado hawajapata mbolea.

“Eneo hili letu la Marioshoni ni ghala la chakula katika Jimbo la Nakuru, tunakuza aina zote za mboga, karoti, viazi mahindi na hata ngano. Kwa sasa tatizo letu ni kwamba wakulima wa hapa hawajanufaika na mbolea kutoka kwa Serikali,” alisema Joseph Kiprotich, mmoja wa wakaazi hao.

Aidha Mwakilishi wa Wadi ya Marioshoni Agnes Cherotich Salim amesema ametoa mapendekezo katika Bunge la Jimbo hilo ili kunusuru wakulima ambao wanaendelea kulalamikia Serikali kusawazisha mgao wa mbolea.

Salim ameuliza Serikali kufungua kiwanda hicho katika Wadi yake akisema wakulima wanalazimika kununua pembejeo kwa bei ya Sh3,500 kwa mfuko wa kilo 50 badala ya kunufaika na mbolea ya Serikali inayouzwa kwa bei ya Sh1,800.

Mwakilishi huyo alisema kuwa huenda usalama wa chakula katika Jimbo la Nakuru ukaathirika baada ya kuchelewa kwa msimu wa upanzi jambo ambalo limechangiwa na kiangazi.