Wakaazi wa eneo la Kinyui wamemtaka gavana wa kaunti ya Machakos Dkt Alfred Mutua awajengee choo katika soko la Kinyui.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katika mazungumzo na wakaazi hawa, walidai kuwa choo cha umma kilichokuwa kikitumiwa na wananchi kilibomolewa na watu waliokuwa wakitengeneza barabara ya kutoka Tala kwenda Kinyui chini ya serikali ya kaunti hio mwaka juzi. 

Tangu siku hiyo, wakaazi hawa na hasaa wafanyibiashara wamekuwa wakihangaika na kulazimika kujisaidia vichakani kutokana na ukosefu wa choo cha umma katika soko hilo. 

Aidha, walidai kuwa wamekuwa wakiwasilisha shida hio lakini haijawahi kushughulikiwa, pale walitaka gavana huyo awajibike vilivyo. 

"Sisi kama wafanyabiashara katika Soko hili, huwa tunapatwa na wakati mgumu katika shughuli zetu za kufanya kazi kwani kutokana na ukosefu wa vyoo huwa tunalazimika kujisaidia vichakani kwani vyoo vingi vya nyumba za kupanga katika Soko hili huwa na viful, " alisema Mercy Kyuma mfanyibiashara katika soko hilo.

Isitoshe, walimtaka gavana huyo amalize kutengeneza barabara hio ya kutoka Tala hadi Kinyui kwani ilitengenezwa kufikia nusu huku sehemu iliyotengenezwa kuanza kuharibika.