Wakaazi na wafanyi biashara katika mji wa Kisii wameonywa dhidi ya kuwaajiri watoto wadogo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa watoto wengi wanaajiriwa kwenye mashamba, hoteli, maduka na kama wafanyi kazi wa nyumbani kinyume cha sheria.

Akizungumza kwenye afisi yake, waziri wa viwanda na biashara kwenye kaunti ya Kisii Ibrahim Moiro alisema ni kinyume cha sheria kuwajiri watoto hasa wa shule.

“Ni jambo la kushangaza kuwa hata baada ya ajira ya watoto kupigwa marufuku kumekuwa na ongezeko la ajira ya watoto kinyume cha sharia,” alisema.

Aliongezea kuwa huu ukiwa ni wakati wa likizo, kuna visa vingi vya ajira ya watoto kwa sababu ya lindi la umaskini hujipata hawana chaguo.

Halikadhalika, amewataka wazazi kuwajibika na kuwashauri watoto wao dhidi ya athari ya za ajira ya watoto.

“Nawaomba wazazi wawajibike na kuwashauri watoto wao dhidi ya ajira ya watoto,” alisema.

Aidha, amewaonya wanaoendeleza tabia hii kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.

“Sheria kali itachukuliwa kwa wale watakaopatikana wakikiuka sheria hii,” alisema hukku akiwaomba washikadau wa elimu kuingilia kati, na kuwasihi watoto kutumia likizo hii kujinoa kimasomo badala ya kuharibu wakati wao wakitafuta kazi.

Huku likizo ya muhula wa kwanza ikiwa bado inaendelea, kumekua na ongezeko la ajira ya watoto kwenye mashamba, mikahawa na maeneo ya burudani kinyume cha sheria.