Kamishna wa kaunti ya Uasin Gishu Abdi Hassan amewahakikishia wakaazi kuwa usalama umeimarishwa haswa wakati huu ambapo wengi wao watakua wakisherehekea siku kuu ya krismasi na mwaka mpya.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya sherehe za Jamhuri katika uwanja wa 64 mjini Eldoret, kamishna huyo alisema kuwa wananchi wasiwe na hofu kwani maafisa wa usalama wamewekwa tayari kuhakikisha usalama upo shwari.
"usalama uko imara katika kaunti hii, na ningependa kuwasihi wananchi kuwa huru kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kuhusiana na wanaopanga kuvuruga usalama," alisema Hassan.
Aidha, aliwasihi madereva wa magari kuwa makini barabarani ili kuepuka ajali.
"Maafisa wa trafiki pia watakuwa makini ili kukabiliana na wale wanaokiuka sheria za barabarani," alisema Hassan.