Wakaazi wa jumba moja viungani mwa mji wa Kisii Daraja Moja karibu na ofisi za kampuni ya Pikipiki za Honda wamehama kwa dharura baada ya jumba hilo kuanza kuzama.
Kulingana na wakaazi hao jumba hilo kwa jina Storm Apartment lilionyesha dalili ya kuporomoka leo asubuhi baada ya kutokea tetemeko la ardhi jana usiku jambo ambalo lilisababisha wengi kuanza shughuli ya kulihama jumba hilo.
Juliet Musumba ambaye ni mmoja wa wakaazi wa jumba hilo alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakiendelea kuhama nyumba hiyo.
"Jana kumekuwa na tetemeko la ardhi nilikuwa kazini nilipoitwa na kuambiwa kuwa watu wanahama kwa sababu jengo tunamoishi lina dalili ya kuporomoka,” alisema Musumba.
Mkaazi mwingine ambaye alijitambulisha kwa jina Abdi, alisema kuwa hilo jumba lilionyesha dalili za kuzama baada ya tetemeko la ardhi jana usiku na kuongeza kuwa mmliki wa jumba hilo pia alichimba kisima kipana chini cha kuhifadhi maji ambacho alidai huenda kilichangia kwa njia moja au nyingine kwa kuzama kwa jengo hilo.
'Hatuna uhakika na usalama wetu haswa baada ya jengo hili kuonyesha dalili ya kuanguka, ndio maana hatuna budi ila tu kuondoka kwa usalama wetu,” aliongezea Abdi, mkaazi.
Jumba hilo ambalo linadaiwa kuwa la mmoja wa wamiliki wa Hoteli kubwa ilioko mjini Kisii lilijengwa hivi karibuni na halijamaliza hata mwaka mmoja.
Hata hivyo kwa mara ya kwanza Maafisa wa Polisi pamoja na wale wa zimamoto na huduma za uokozi walikuwa pale mapema kusaidia iwapo kutatokea na dharura.
Mpaka wakati tukiyaandika makala haya vijana ambao walikodishwa na wakazi wa jumba hilo walikuwa bado wanashusha mali yao kutoka orofa ya juu huku wakisononeka kufuatia hali hiyo ya dharura iliyowapata.