Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Hatua ya sanamu ya mamba iliyokuwa na umaarufu mjini Mombasa kuharibiwa imeibua hisia mbalimbali miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo.

Sanamu hiyo iliyokuwa katika shamba la Mamba Village iliharibiwa siku ya Jumanne ili kutoa nafasi kwa upanuzi wa barabara.

Shamba la Mamba Village lina umaarufu sana kwa vile wageni mbalimbali huzuru sehemu hiyo kuona mamba na kujifurahisha kwa michezo tofauti.

Sanamu hiyo ya mamba iliyokuwa katika lango kuu la bustani hiyo inadaiwa kutengezwa na mchoraji kutoka taifa la Israel miaka 41 iliyopita.

Sanamu hiyo pia ilikuwa kivutio kikubwa katika shamba hilo huku likitumika kama nembo ya kutambulisha eneo hilo sio tu kwa wakaazi, bali hata kwa wageni.

Ubomozi wa sanamu hiyo umeibua hisia mseto huku wakaazi na hata viongozi katika Kaunti ya Mombasa wakikosoa hatua hiyo.

Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano, baadhi ya wakaazi wameitaka idara ya makavazi kuingilia kati swala hilo.

“Mimi nadhani idara ya makavazi inafaa kuingilia kati kwa sababu inahusika na uhifadhi wa maeneo ya kihistoria na kuyalinda kutokana na uharibifu wa aina mbalimbali. Sehemu kama ile tumeitambua kwa miaka mingi sana,” alisema Athman Said, mkaazi wa Mombasa.