Wakaazi wa lokesheni ya Nyabisimba, iliyoko katika wadi ya Bonyamatuta eneo bunge la Mugirango Magharibi wameomba kubadilishiwa madaktari kwa kile wanachosema kuwa ni utowajibikaji wa madaktari hao kila siku.
Wakiongea na mwandishi huyu wa habari mnamo siku ya Jumatatu, wakaazi hao walisema kuwa madaktari hao hufika kazini mwendo wa saa tano au saa sita mchana, ilihali wengi wao huwatangulia wakiwa na nia ya kuhudumiwa kwa wagonjwa wao.
“Mimi mwenyewe nilikuwa na mgonjwa nikafika hapa saa tatu asbuhi, hakuna daktari na nimeshindwa cha kufanya. Tunaomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kuangalia suala hilo maana tunasumbuka sana hata mgonjwa anaeza fariki bila kuhudumiwa,” aliohoji Mellen Bosibori, mkaazi aliyekuwa na mgonjwa.
Wakati uo huo, wakaazi hao walipendekeza kuwa heri madaktali kubadilishwa ili kuona kama mabadiliko yatafanywa kwa kufika mapema ili wagonjwa kuhudumiwa.
“Hii leo si mara ya kwanza madaktari kuchelewa, wamezoea sana, sasa tunahitaji tubadilishiwe madktari wengine, kama sivyo warekebishe na wawe wakifika hapa mapema, hilo ndio tunahitaji,” alisema Meshack Chomo, mkaazi mwengine pia aliyekuwa na mgonjwa.
Sasa kibarua ni kwa serikali ya kaunti ya Nyamira kusikia kilio cha wakaazi hao, maana hawaoni kama wanashughulikiwa kulingana na mahitaji yao.
“Tumesubiri kuona hatua ikichukuliwa na serikali ya Nyamira kwa majuma mawili yajayo, maana tunaendelea kusumbuka sana,” aliongezea Bosibori.