Wakaazi, wasafiri na watalii kwa jumla wamelalamikia moshi wa sumu unaotoka katika jaa la Kibarani.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakaazi hao walisema kuwa taka hizo zinapochomwa, hutoa moshi ambao unaweza kuwadhuru kiafya.

Madereva wanaotumia barabara hiyo kutoka Nairobi na maeneo ya Kaloleni na viunga vyake, wamesema kwamba kando na kuwa tishio kwa afya yao, moshi huo huwa unasababisha ajali kwa kuwa hawawezi kuona mbele vizuri.

"Mwezi uliopita, kulikuwa na ajali mbili kwasababu ya moshi huu. Madereva hupoteza uwezo wa kuona mbele unapoingia mjini kupitia mteremko wa kibarani,” alisema Daniel Otiende, dereva wa matatu.

Watalii pia wamelalamikia hali hiyo, kwa kusema kuwa hao hulazimika kupumua hewa hiyo chafu wanapokamwa katika msongamano wa magari wakati wa asubuhi na jioni.

"Watalii tunaowabeba kutoka Uwanja wa ndege wa Moi hulalamikia moshi huo, ambapo sisi hulazimika kuwaambia kuwa serikali ya kaunti itashughulikia swala hilo,” alisema Abed, dereva wa teksi za kibinafsi.

Hata hivyo, serikali ya kaunti imekana madai hayo.

"Madai ya kuwa kuna moshi wa sumu maeneo ya Kibarani ni uwongo mtupu,” alisema katibu wa kaunti, Bwana Francis Thoya.

Kaunti ya Mombasa huzichoma taka zinazokusanywa mjini katika jaa la Kibarani, ambapo familia nyingi maskini huokota chupa za plastiki ili kujikimu kimaisha.