Wakaazi katika eneo la Buxton, Kaunti ya Mombasa, wameitaka serikali ya kaunti kushughulikia swala la kuwepo kwa mrundiko wa taka katika eneo hilo.
Wakaazi hao wameitaka idara husika kushughulikia swala hilo kwa haraka na kuhakikisha kuwa taka hizo zinazolewa kwa wakati ufaao ili kuzuia kuzuka kwa mkurupuko wa magonjwa.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi katika eneo hilo, wakaazi hao, wakiongozwa na Kelvi Omondi, walisema kuwa shida hiyo inaathiri shughuli zao za kujitafutia riziki.
“Harufu mbaya inayotoka kwa taka hizo hutufanya sisi kama wafanyibiashara kukosa wateja katika eneo hili, kwa kuwa wengi wao huwa ni watu ambao husubiri kuabiri gari katika kituo hiki,” alisema Omondi.
Aidha, wameitaka serekali ya kaunti kufuatilia swala hilo na kupata suluhisho la kudumu kwa wakaazi hao.
Wakaazi hao walisema kuwa wametembelea afisi za serikali ya kaunti mara kadhaa huku kila mara jibu wanalolipata kutoka kwa maafisa hao likiwa ‘kuweni na subira swala hilo linashughulikiwa’.
Abdi Hassan, mmoja wa abiria huabiri gari katika kituo hicho, alisema kuwa uvundo unaotoka kwa taka hizo umekuwa kero sana na kuitaka serikali ya kaunti kuwajibikia majukumu yake.