Wakaazi wa Mavoko wanahofia kuzuka kwa mkurupuko wa maradhi kutokana na takataka kujaa katika eneo hilo.
Kulingana na wakaazi hao, magari ya halmashauri ya jiji yanayofaa kuzoa taka hayajaonekana kwa muda mrefu, hatua iliyosababisha taka kujaa na kutapakaa kila mahali.
Wakaazi hao walisema kuwa wanalazimika kuwalipa watu ili kuzoa takataka hizo kutumia mikokoteni na kuitaka serikali ya kaunti kuwajibika ipasavyo.
Akizungumza siku ya Jumatatu na mwandishi huyu, msimamizi wa kaunti ndogo ya Mavoko Bwana Onesmus Ituo, aliwalaumu wapangaji wa ploti katika eneo hilo kwa kutupa taka ovyo.
Bwana Ituo alisema kuwa wenye nyumba za kupangisha hawana mahala palipotengwa pa kutupwa taka, na hivyo kuwasababisha wapangaji kutupa taka ovyo.
"Wenye nyumba za kupanga wangekuwa na mahala palipotengwa pa kutupa taka, labda kazi ya kuzoa taka ingekuwa rahisi,” alisema Ituo.
Haya janajiri siku mbili baada ya Mbunge wa Mavoko Patrick Makau kuwaongoza wakaazi katika hafla ya kusafisha maeneo kadhaa katika kaunti hiyo ndogo.