Wito umetolewa kwa Idara ya uvuvi, Kaunti ya Kisumu, kuingilia kati ili kutatua mzozo kati ya wanadamu hasusan wavuvi, na mamba katika ufuo wa Ziwa Victoria, eneo la Ugunja.
Haya yanajiri baada ya kijana mmoja, Evans Okinyi, kuvamiwa na mamba katika ufuo huo, huku akinusuriwa na wavuvi wenzake kutoka kwenye ndimi za mauti.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, kijana huyo aliyeachwa na majeraha katika mguu wake wa kushoto, alivamiwa na mamba huyo akiwa katika shuguli zake za uvuvi.
“Ilibidi wenzake waliokuwa wanavua samaki kutumia vifaa mbali mbali kumgonga mamba huyo ili apate kumwachilia kijana huyo. Okinyi anaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya rufaa na mafunzo ya Nyanza,” alisema Victor Ouma, msemaji wa wavuvi katika ufuo huo.
Ouma pamoja na wakaazi wa eneo hilo wamedokeza kuwa visa vya uvamizi wa mamba vimekithiri katika eneo hilo, huku watu watano wakiuawa na mamba.
Wakaazi hao walidai kuwa licha ya kuwasilisha lalama zao katika idara husika, hakuna hatua zilizochukuliwa.
''Tumepeleka malalamishi yetu katika afisi ya fisheries lakina hakuna hatua imechukuliwa na viongozi wetu akiwemo mwakilishi wadi wa eneo hili,” alisema Ouma.