Mkuu wa polisi mjini Mombasa Lucas Ogara amewataka wenyeji wa maeneo mbalimbali kutoshiriki mikutano inayoandaliwa bila idhini kutoka kwa idara ya polisi.
Akizungumza baada ya maafisa wa polisi kuutibua mkutano uliokuwa umeitishwa na kundi moja la viongozi wa Kiislamu, Ogara aliwataka wakaazi kuhakikisha kuwa wanaoitisha mikutano wana vibali kabla ya kuanzisha mikutano yao.
Mkutano huo ulioitishwa ili kuwahamasisha Waislamu kuhusu utangamano baina ya dini mbalimbali, ulitibuliwa baada ya maafisa wa polisi kupata habari kutoka kwa idara ya ujasusi kuwa viongozi hao hawakuwa na idhini yoyote.
Aidha, ilisemekana kuwa viongozi hao walifahamu kuwa ni kinyume cha sheria kwa mikutano yoyote kuandaliwa bila ya ruhusa kutoka kwa serikali.
Kulingana na Ustadhi Shaban Mwalimu, ambaye ni mmoja wa viongozi waliokuwa wamefika kwenye mkutano huo, mkutano huo haukuwa na nia mbaya kwani ulinuia kujadili utangamano na uwiano baina ya dini mbalimbali katika eneo la Pwani.
Hata hivyo, Ogara alisema kuwa watafuatilia kwa karibu kundi hilo kama litafanya mkutano mwengine bila ya idhini.
Alisema kuwa viongozi wa kidini pia wanapaswa kupata idhini kutoka kwa serikali kabla ya kuitisha mikutano.