Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imetoa onyo kwa watu wenye tabia ya kujaribu kujitoa uhai katika kivuko cha feri cha Likoni.
Akizungumza siku ya Jumanne katika kivuko hicho mjini Mombasa, afisa mkuu wa polisi eneo la Likoni Willy Simba alisema kuwa atakayepatikana atachukuliwa hatua za kisheria.
Simba alisema kuwa tabia hiyo imeonekana kuzidi katika kivuko hicho, na tayari maafisa wa polisi wametumwa kushika doria katika eneo hilo kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote anayejaribu kujitoa uhai.
Afisa huyo alisema kuwa kivuko hicho hutumiwa na watu wengi hasa watalii, na hatua hiyo huenda ikawatia hofu na kuaathiri sekta ya utalii.
Simba amewataka wakaazi kuzingatia maisha yao pamoja na kutafuta njia mwafaka ya kusuluhisha matatizo yao.
"Tunatoa onyo kwa wale walio na tabia ya kujaribu kujitoa uhai katika kivuko cha feri cha Likoni. Ikiwa mtu anakumbwa na matatizo fulani, sharti apige ripoti kwa maafisa wa polisi ili swala hilo lisuhulishwe,” alisema Simba.
Haya yanajiri baada ya kijana mmoja mwenye umri wa miaka 20 kujaribu kujitoa uhai katika kivuko cha feri cha Likoni siku ya Jumatatu.