Wakaazi wa mtaa wa Maili Sita katika eneo bunge la Bahati wameonywa dhidi ya kujichukulia sheria mikononi mwao kwa kuwavamia na kuwachapa wagemaji wa pombe haramu.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Chifu mkuu wa lokesheni ya Kiamaina Arnold Mwangi, amewataka wakaazi hao badala yake kushirikiana na polisi na utawala wa mikoa katika kuangamiza biashara hiyo ambayo imekithiri katika eneo hilo.

Akiongea katika afisi yake leo asubuhi Maina alisema kuwa ni makosa kwa raia kuvamia maboma ya watu na kuwachapa watu wanaodhaniwa kuwa wagemaji.

Akitoa mfano wa hapo jana ambapo kundi la kina mama walivamia boma la mgemaji mmoja na kuteketeza mali yake, Maina alisema haiwezekani kutatua shida kwa kutumia njia zinazovunja sheria.

“Tunakubali kuwa tuna shida ya pombe haramu katika eneo hili lakini pia hatuwezi kuvunja sheria kwa kisingizio kuwa tunapigana na pombe haramu.Ni makosa kuvamia boma la mtu na kuharibu mali yake hata kama ni mgemaji,ningependa kuwarai raia kutumia njia za kisheria katika kupigana vita dhidi ya pombe haramu na mimi kama chifu niko tayari kushirikiana nao lakini lazima tufuate sheria,” alisema Maina.

Maina aliwakumbusha raia kuwa wanaweza wakashtakiwa kwa kuvamia boma la mtu na kuharibu mali yake hata kama walikuwa wanapigana na pombe haramu.

Onyo la chifu huyo liliwadia baada ya mama mmoja kuchapwa na kundi la kina mama hapo jana waliomshtumu kwa kuwaharibu mabwana zao kwa kuwauzia pombe haramu.