Wakaazi wa Mombasa wamepongeza pendekezo la kufukuliwa kwa miili ya wapiganaji wa Mau Mau wanaoaaminika kuzikwa katika Gereza la Kamiti ili kufanyiwa mazishi ya kiheshima.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika eneo la Likoni, wakaazi hao, wakiongozwa na Saidi Hassan, walisema kuwa wapiganaji hao wanafaa kupewa heshima kubwa ikizingatiwa walichaangia pakubwa katika kupatikana kwa uhuru wa taifa.
Aidha, wakaazi hao waliongeza kuwa serikali inafaa kuwafadhili na kusimamia maisha ya familia za wapiganaji hao.
Hatua hii inajiri baada ya Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga, kuihimiza serikali kuanzisha shughuli ya kufukua miili ya wapiganaji wa Mau Mau wanaoaminika kuzikwa katika Gereza la Kamiti ili wapokee mazishi yenye taadhima.
Dkt Mutunga alisema serikali yapasa kutafuta mabaki hayo kwani wapiganaji hao walichangia pakubwa kupokea uhuru wa nchi hii.
Akizungumza wakati wa kukabidhi faili ya kesi na rufani ya marehemu Dedan Kimathi kutoka Uingereza kwa mashujaa wa Mau Mau katika eneo la Freedom Corner la bustani ya Uhuru, jaji mkuu alisema Uingereza yapasa kufahamu kule Kimathi alizikwa kwani wao ndio waliohusika na kifo chake wakati wa enzi wa ukoloni.
Aidha, Dkt Mutunga alisema serikali yapasa kubuni tume ya kuchunguza na kuwatambua wapiganaji halisi wa ukombozi wa nchi hii na kuwafidia.
Kwa upande wake, katibu mkuu wa chama cha wapiganaji wa Mau Mau, Gitu wa Kahengeri, alisema serikali yapasa kujenga mnara wa kuwaenzi wa kuwakumbuka wapiganaji wa ukombozi.
Faili ya Dedan Kimathi ilipokewa kutoka maktaba ya bunge la Senate ya chuo kikuu cha London mwezi uliopita.