Kulizuka kisanga Ijumaa katika wadi ya Viwandani mjini Naivasha baada ya wakazi kuzua rabsha na vurumai wakati wa mkutano uliokuwa umeitishwa kujadili mipango kadhaa ya maendeleo chini ya serikali ya kaunti.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi waliojawa na gadhabu aidha walisimamisha mkutano huo wakisema kuwa miradi iliyokuwa imetengewa pesa haijafanyika licha ya kuwa pesa hizo zimetumika.

Tukio hilo lilimlazimu msimamizi wa kaunti ndogo ya Naivasha Julius Nyaata kuondoka kwa lazima huku wakaazi hao wakimkemea vikali.

“Wakati umefika kwa Wakenya kuambiwa ukweli kuhusu pesa zao, hatutaki tena mambo ya kusomewa vitabu, tunataka vitendo sasa, akafoka kwa hasira mkaazi Justus Kamau.

Aliyekuwa meya wa mji huo Gikonyo Mariku alidai MCA wa eneo hilo Eunice Mureithi amefuja pesa za kaunti hiyo.

Mariku amesema kuwa bi Mureithi anayejulikana kama Mama Soko alikuwa amenakili kuwa amejenga darasa la chekechea katika shule ya msingi ya Naivasha DEB, mradi ambao haujafanyika hadi wa sasa.

“Hakuna darasa limejengwa kama ambavyo tunaambiwa, je pesa hizi shilingi milioni mia tatu, zilienda wapi? Mama soko amezifuja” akasema Gikonyo ambaye pia ni mwenyekiti wa shule hiyo ya Naivasha DEB.

Naye kiongozi wa vijana Mwangi Muraya amesema kuwa sheria ilikuwa bayana kuwa ili mradi wowote ufanyike, ni sharti wakaazi wahusishwe, huku wakimshtumu gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua kwa kukosa kuwajibika.

MCA Eunice hakuwa kwa mkutano huo, na hakupokea simu za mwandishi huyu.