Wakaazi wa kitongoji duni cha Otongolo viungani mwa mji wa Kisumu wamelalamikia ukosefu wa usalama katika eneo hilo ambapo wamedai wanahangaishwa na genge la vijana wanaowavamia majumbani mwao usiku na kuwaibia kimabavu.
Wakaazi hao wamelalamikia kisa cha hivi majuzi ambapo baadhi ya vijana walivamia boma moja na kuiba bidhaa za nyumba wakati wenye boma hilo walipokua safarini kwa muda na kisa kingine cha mama mfanyibiashara kushambuliwa jioni alipokua akirejea nyumbani kutoka sokoni.
Wakitoa lalama hizo kwenye baraza la Naibu wa Chifu eneo hilo siku ya Jumatano, wakaazi hao waliwataka Maafisa wa utawala kulishughulikia swala hilo kwa dharura na kuweka mikakati dhabiti ya kuimarisha usalama katika eneo hilo siku zijazo.
“Bwana Naibu Chifu sisi tumechoshwa na kuvamiwa na mali yetu kutwaliwa kimabavu. Tunaomba utusaidie ili tuwe na usalama wa kutosha manyumbani mwetu na hata vijijini tunakovamiwa na magenge ya vijana ambao hurandaranda bila kazi,” alisema Lucy Akinyi mmoja wa wafanyibiashara eneo hilo ambaye pia alishambuliwa majuma mawili yaliyopita.
Walisema kuwa wanajua vyema kuwa wanaowahangaisha sii wengine bali ni vijana ambao waliacha shule na hawana vibarua, wakisema kuwa kazi yao ni kushinda wakikaa kando ya barabara na kupanga njama za maeneo watakayovamia usiku.
Naibu wa Chifu, Wilson Outa aliwahakikishia wakaazi hao kuwa swala hilo litashughulikiwa kikamilifu, akitangaza msako mkali kuanzishwa ili kuwanasa wahalifu wote.
“Tumepata ripoti hizi mara kwa mara na vyombo vyetu vya usalama vimeanza kuwajibika ambapo kila mmoja wa wahalifu hao atanaswa na kukumbana na makali ya sheria,” alisema Outa.