Mbunge wa Nakuru Magharibi Samuel Arama alijipata pabaya Alhamisi baada ya kukosa kutimiza ahadi ya soda kwa wakaazi wa Ingobor katika hafla ya harambee. Inadaiwa kuwa mbunge huyo alikuwa ameahidi kununulia wakaazi soda na maji ya kunywa wakati wa hafla ya harambee eneo hilo.
Hata hivyo, alibadili msimamo wake nyakati za mwisho na kusema kuwa hatahudhuria mkutano huo wa mchango kusaidia mradi wa maji.
"Arama alikuwa ametuahidi soda lakini amefika dakika ya mwisho na kugeuka,"alisema mmoja wa wakaazi.
Inaarifiwa kwamba mbunge Arama alisusia mkutano huo kutokana na hatua ya mpinzani wake wa 2017 David Karuri kuhudhuria mkutano huo.
Karuri ametangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge Nakuru Magharibi ambacho kwa sasa kinashikiliwa na Arama.
Ilimlazimu mwakilishi wadi ya Kapkures Joseph Lang'at kuingia mfukoni na kununua soda pamoja na maji ya kunywa.