Wakaazi wa lokesheni za Gesima na Mochenwa eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira, wamewaomba machifu pamoja na manaibu wao kuwachukulia hatua kali za kisheria washukiwa wote wa wizi ambao wametajwa kusumbua wananchi maeneo hayo.
Wakiongea katika mkutano wa usalama uliofanyika katika sehemu ya Matunwa, wadi ya Gesima uliowaleta wakaazi wa lokesheni hizo mbili pamoja ,chifu wa lokesheni ya Gesima, Ogeto Osong’o na mwenzake wa Mochenwa Magara Makori, waliwaahidi wakaazi hao kuwa watashirikiana pamoja kuwachukulia wote waliotajwa kuwa washukiwa wa wizi hatua kali za kisheria.
Wakaazi walitoa orodha ya washukiwa 11, kutoka kwa lokesheni hizo na kuwaomba machifu kawachukulia hatua kwa haraka kwa kuwa wamechoshwa na vitendo vya wezi hao.
Haya yote ni kutokana na kuibwa kwa ng’ombe ya mzee Zephania Ondicho na duka nyingi kuvujwa na kuporwa mali katika eneo hilo.
Kwingineko wenye magari wameonywa kwa kudaiwa kuwa huenda ng’ombe hizo hubebwa na magari hayo huku wananchi wakiapa kuwa mwenye gari lolote litakalopatikana kuhusika atachukuliwa hatua kali.
“Hata usiku hatulali kwa kuwa tunalinda ng’ombe wetu kwa hofu kuwa wezi hao wataweza kuja na kuiba. Hii imefanya watu kutofanya kazi nyingine wakati kumekucha kwa kuwa mtu huwa na uchofu na uzingizi,” alihoji Kalvin Barongo, mkaazi.
Chifu hao kwa sasa wamesema watawaandikia washukiwa hao wote barua na kuwaagiza wafike katika ofisi zao ili kujitetea kutoka kwa shutuma hizo na kama watapatikana kuwa na hatia watachukuliwa hatua kali ya kisheria.
“Tutawandikia washukiwa hao wote barua za kuwaagiza kufika ofisi zetu, barua hizo watapatiwa na manaibu wetu. Pindi watakaporipoti, watatusaidia kwa uchunguzi zaidi,” alihoji Ogeto.