Wakazi wa tarafa ya Turi, Kuresoi pamoja na Wadi pana ya Nyota wamelalamikia kuhangaishwa na wezi wa mifugo ambao wamekuwa wakivamia boma zao wakiwa wamejihami kwa silaha hatari  nyakati za usiku na kuiba Ng’ombe.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wamesema licha ya kuwepo kwa maafisa wa kukabiliana na wezi wa mifugo na wale wa utawala (AP) katika wilaya hizo mbili bado wezi wa mifugo wanaendelea kuhangaisha wenyeji.

Usiku wa kuamkia jumatatu wakazi wa Shamba la kwa Wira walimpiga mshukiwa mmoja wa wizi wa mifugo ambaye alifumaniwa akiwa kwenye zizi la ng’ombe huku wenzake wawili wakitoroka.

Wakaazi hao wamesema wezi wa ng’ombe wanawatia hofu kubwa jambo ambalo huenda likavuruga uwepo wa Amani.

Uchunguzi wetu umeonyesha baadhi ya wafugaji wanatumia chumba kimoja na mifugo hali ambayo inadhihirisha wasi wasi walionao huku usalama ukiendelea kudorora.

Wamesema wamekuwa wakikesha nje, pamoja na kuunda makundi ya usalama vijijini kuona washukiwa wa wizi wa mifugo wamekamatwa ama mifugo waliowaiba wamerejeshwa.

Wakaazi hao wamesema ni jambo la kukera kuona wakazi wakitumia chumba kimoja na mifugo katika maeneo ambayo serikali imetuma maafisa wake kutumikia wakazi.

Wamemtaka mkuu wa wilaya hiyo Silas Gatobu kufanya vikao vya Amani pamoja na kuwatuma maafisa zaidi wa usalama katika maeneo ambayo wizi wa mifugo umefikia viwango vya kuogofya.