Mwakilishi wa wadi ya Bahati katika kaunti ndogo ya Nakuru Kaskazini, amesema “nitapiga siasa usiku kama ni lazima, kwa sababu mchana niko mashinani nikichapa kazi”.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Peter Nderitu Mwangi alikuwa akizungumza na wakaazi wa kijiji cha Kamiruri ambapo alikuwa akisimamia ufunguzi wa barabara ambayo haijawahi kuchimbwa kutokana na kupita kwenye milima na mabonde.

Barabara hiyo inayotoka kituo cha kibiashara cha Bahati hadi maili Kumi na Mbili kwenye barabara ya Solai, itakuwa ni afueni kwa wakaazi hao ambao walikuwa wakizunguka umbali wa kilomita sita kufika kituo hicho cha kibiashara.

Nderitu alisema baada ya tinga tinga la kaunti kuchimba barabara hiyo yenye kilomita 3.5, itawekwa changarawe ili kufanya magari ya uchukuzi wa abiria yaweze kukwea milima iliyobaki.

“Watu wanaeneza siasa kwamba serikali yetu hafanyi kazi. Nataka kuwaambia nitapiga siasa usiku kama ni lazima, kwa sababu mchana niko mashinani nikichapa kazi, kuchimba barabara na kuweka maji, kati ya miradi mingine. Ningependa wale wote wanaokuja kuwaambia kwamba wanataka kuchaguliwa, mtu aonyeshe amefanya nini kwanza,” alisema Nderitu.

Wakaazi hao walielezea kufurahishwa kwao na ukarabati huo.

“Sasa hata kuchimba mitaro ya mifereji imekuwa rahisi kwa sababu tumetengenezewa barabara ambayo haijawahi kuchimbwa tangia uhuru 1963,” Jane Kamau alisema.